Kocha mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet, ameukosoa mpangilio mzima wa Ligi ya soka ya Tanzania Bara uliopangwa na Shirikisho la Kandanda nchini Tanzania TFF akidai kwamba mpangilio haujapangwa kwa haki.
Alilalamikia kitendo cha timu yake kupangiwa mechi mbili mfululizo za ugenini mapema mwanzoni mwa ligi wakati wapinzano wao Simba watacheza mechi zao mbili za mwanzo wakiwa nyumbani.
"Mechi yetu ya kwanza tutacheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kisha tutaenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar wakati Simba watakuwa wakicheza nyumbani. Nadhani hii siyo haki, ingepaswa mechi moja iwe nyumbani na nyingine ugenini." Alisema kocha wa Yanga.
Yanga wanatarajiwa kuianza ligi kwa kupambana na Tanzania Prisons ambao wamepanda daraja tena msimu huu kwenye uwanja wa Sokoine huko Mbeya Septemba 15, na kisha watasafiri kwenda Morogoro kupambana na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri siku nne baadaye.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba, watakutana na African Lyon kwenye mechi yao ya ufunguzi itakayopigwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam Septemba 15 kabla hawajakutana uso kwa uso na Ruvu Shooting Stars Septemba 23 kwenye uwanja huohuo wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment