Chadema wamelezea mashaka yao makubwa juu ya tume ya watu watano iliyoundwa na waziri wa mambo ya ndani Dr. Emmanuel Nchimbi ili kuchunguza nini kilisababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Iringa aliyekuwa mwakilishi wa Chennel Ten Bwana Daudi Mwangosi siku ya Jumapili.
Akiongea na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Chadema, Mkurugenzi wa sheria, katiba na haki za binadamu Bwana Tundu Lisu, aliishambulia tume hiyo kwa madai kwamba baadhi ya wajumbe hawana sifa.
Lakini waziri Nchimbi yeye alisema, "Ninachosubiria hivi sasa ni taarifa toka kwa tume juu ya nini kilisababisha mwandishi auawe. Sitakaribisha hoja yoyote juu ya kuundwa kwa tume." Alisema.
Lakini Bwana Tundu Lisu ambaye ni mwanasheria alimtaja Jaji, ambaye ni mwenyekiti wa tume iliyoundwa na waziri, Jaji Stephen Ihema, kwamba hana sifa za kuiongoza tume hiyo Akidai kwamba tume imeundwa kwa kuzingatia urafiki na kwamba hili litasababisha kutokuwepo kwa uchunguzi huru.
Lisu aliongeza kusema, "Mambo yote yako wazi kwa jamii, tunachohitaji ni maafisa wa juu wakiwemo waziri na Inspekta Jenerali wa Polisi wachunguzwe iwapo walitoa amri ya mauaji."
Alisema kuwa wengi wa wajumbe hawana ufahamu wa kazi hiyo na kumuomba Rais Jakaya Kikwete aunde tume mpya itakayojumuisha Majaji wa mahakama ya rufaa hata wa mahakama kuu lakini asiwepo Jaji Ihema.
Aliongeza kusema kuwa Chadema wangependa kuona Dr. Nchimbi akionesha ukomavu wa kisiasa kwa kujiuzulu ama vinginevyo rais amfukuze kazi.
Wewe msomaji unasemaje kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari pamona na tume iliyoundwa na waziri Nchimbi?
Thursday, 6 September 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment