Yanga Yarudisha Tano bila Simba
Nukuu Toka Gazeti la MwanaSpoti:-
SIMBA imefanya makosa matano na Yanga ikayatumia kikamilifu kumwondoa beki mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbuyu Twite kutoka Msimbazi na kumvalisha jezi ya Mtaa wa Jangwani.
Twite alisaini mkataba na Simba mapema mwezi huu mbele ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, jijini Kigali, Rwanda na jezi yake namba 4 kutambulishwa katika tamasha la Simba Day ndani ya Uwanja wa Taifa, Agosti 8 ingawa mchezaji husika hakuwapo uwanjani hapo.
Baada ya Simba kutangaza kumnasa beki huyo, Yanga kupitia kwa mmoja wa viongozi wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin Kleb, aliiambia Mwanaspoti kwamba lazima ajibu mapigo kwani Simba imemdhalilisha kwa kusema imemgaraza kwenye sakata la kumnasa Twite katika filamu inayoitwa 'Eights Hours In Kigali'.
Kulipa kisasi huko kulitimia baada ya Ijumaa iliyopita, Yanga kutangaza kumsainisha beki huyo kwa kutumia vigezo vitano, idadi ambayo ni sawa na ushindi wa mabao 5-0 ambao Simba iliupata dhidi ya Yanga katika pambano la mwisho la Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Mbaya zaidi ni kuwa Twite aliwatuma viongozi wa APR ya Rwanda na Lupopo ya Congo kurudisha Dola 30,000 (Sh 45 milioni) alizochukua Simba kama utangulizi.
Yanga imetumia upungufu wa maeneo matano makubwa kuizidi kete Simba kwenye usajili wa mchezaji huyo kama ifuatavyo;
Mosi; Kushitukia dili la mkopo. Bin Kleb anadaiwa kumsainisha Mbuyu Twite, Julai 31 kwa makubaliano ya kumpa fedha taslimu Dola 30,000, Siku iliyofuata, Simba ikatua Kigali kumsainisha beki huyo kwa dau la Dola 50,000, lakini wakampa taslimu Dola 30,000.
Baada ya kuelewana na mchezaji hawakwenda kwa APR kujua kama mchezaji huyo alikuwa kwa Wanyarwanda hao kwa mkopo, badala yake Rage akapanda ndege akarudi Dar es Salaam.
Yanga ikabonyezwa na mmoja wa viongozi wa APR na kukimbilia FC Lupopo ya Congo kumalizana nao na kukabidhiwa mchezaji huku ITC yake ikitokea Congo badala ya Rwanda ambako Simba ilishaanza kuiomba.
Pili; Yanga iliongeza dau.
Yanga ilielewana na mchezaji huyo kwa kumpa Dola 30,000 na mshahara wa Dola 2,500 lakini baada ya Simba kuingilia ikabidi waongeze dau hadi kufikia Dola 50,000 (Sh 75 milioni) na wakamkabidhi fedha hizo Twite pale pale huku mshahara ukibaki uleule kama wa Simba.
Tatu; Kukosea jina na sehemu aliyosaini mkataba Simba.
Katika mkataba wa Simba uliochapishwa ukurasa wa tano wa Mwanaspoti leo Jumanne, jina lililotumika kwenye mkataba huo ni Mbuyi Twite wakati mchezaji husika anasisitiza kuwa anaitwa Mbuyu Twite.
Simba ilimsainisha mchezaji huyo jijini Kigali Rwanda lakini kwenye mkataba huo ukurasa wake wa saba imeandikwa kwamba imemsainisha jijini Dar es Salaam, Agosti Mosi.
Nne; Kumwacha Kigali. Rage alifanya kosa kubwa kumsainisha na kumwacha mchezaji huyo jijini Kigali ambako Bin Kleb huenda kila mara kwa biashara zake.
Bin Kleb aliposhtukia kwamba Rage ameondoka kurejea Dar es Salaam kuwahi mkutano wa wanachama pamoja na vikao vya Bunge, akamvaa Twite akiwa sambamba na viongozi wazito wa APR ambao walisaidia kumshawishi.
Tano; Sekeseke la Patrick Mafisango na kutimua wageni.
Yanga ilitua jijini Lubumbashi na kukaa na viongozi wa Lupopo pamoja na mchezaji huyo akiwa sambamba na kaka yake Kabange Twite na kuwalisha sumu kuhusiana na upungufu wa Simba katika utendaji wake.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo, ni kwamba ujumbe wa Yanga uliwaambia Wakongo hao kwamba Simba haikumhudumia vizuri marehemu, Patrick Mafisango licha ya mchango wake aliokuwa nao ndani ya Wekundu hao na kwamba mpaka sasa hata rambirambi hawajatoa.
Jambo ambalo liliwaingia Wakongo hao pamoja na mchezaji husika ambaye yuko karibu sana na dini, hivyo akabadilisha uamuzi. Baada ya pointi hizo tano za nguvu Yanga, haikuishia hapo, ikaendelea kumwaga sumu.
Kuachwa kiholela kwa wageni;
Yanga iliendeleza sumu baada ya kuiambia hata familia ya mchezaji huyo kwamba Simba haina uongozi thabiti na wachezaji wa kigeni huachwa bila kufuata taratibu wakitolea mfano wa Wakongomani Lino Masombo, Kanu Mbiyavanga na Waganda Derick Walulya na Joseph Owino.
Hawakuishia hapo wakaeleza madai ya Kelvin Yondani kwamba viongozi wa Simba wamefoji mkataba wake.
Hadhi ya Yanga;
Umaarufu wa Yanga kwa sasa baada ya kutwaa Kombe la Kagame wiki chache zilizopita pamoja na kupata uongozi mpya ni kati ya sababu pia zilizomlainisha Mbuyu.
Source: MwanaSpoti
0 comments:
Post a Comment